Serikali imetoa wiki moja kwa Mamlaka ya Usimamisi wa Bandari(TPA) mkoa wa Tanga kuhakikisha inarejesha tena matumizi ya mita ya kupimia mafuta (Flow Meters), kabla ya shehena ya meli ya mafuta kutia nanga bandarini hapo.
Hatua hiyo ya serikali inafuatia uamuzi wa TPA kuacha ufungaji wa mita hizo uliofanywa zaidi ya miaka mitano iliyopita ambapo kwa kipindi chote hicho serikali ilikuwa ikiingia hasara na kupoteza mapato.
Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi, Edwin Ngonyani wakati akizungumza katika majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya siku moja iliyolenga kuangalia mwenendo wa utendaji wa Bandari ya Tanga.
Katika ziara hiyo, pia Naibu Waziri alifanya ukaguzi wa Flow meters pamoja na matishari matatu ambayo yamedumu kwa zaidi ya miaka minne bila kufanya kazi bandarini hapo.
Mhandisi Ngonyani alisema serikali imesikia kwamba kufungwa kwa mita za kupimia mafuta(Flow Meters)kwenye bandari za hapa nchini kumetokana na ushiriki wa baadhi ya wafanyakazi wa TPA waliokuwa wamelenga kunufaika kupitia wafanyabiashara wakubwa ambao kimsingi mita hizo zilikuwa zikiwabana katika ulipaji wa kodi.
Pia imeelezwa kuwa baadhi ya wafanyakazi hao wanajihusisha kufanya uchochezi kwa wananchi ambao walitakiwa kupisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya Mwambani, ambao licha ya kulipwa fidia lakini wameendelea kugoma kuachia ardhi hiyo.
“Uamuzi wa kuondoa Flow meters ulikuwa ni wa kipuuzi kabisa na tumesikia uchochezi huu pia ulihusisha baadhi ya wafanyakazi," alisema Ngonyani. "Inasikitisha sana kwani nia yao ilikuwa ni kuwanufaisha wafanyabiashara."
Alisema iwapo watumishi wa TPA wangekuwa na umoja katika kupigia kelele maamuzi yaliyofanywa kipindi hicho, ni dhahiri kuwa hali ya ukwepaji wa kodi kwenye shehena ya mafuta yanayoingia nchini isingefikia ilivyo sasa.
Alisisitiza kwamba serikali itawachukulia hatua za kisheria waliohusika na manunuzi ya matishari matatu kwenye Bandari ya Tanga ambayo hayakidhi vigezo vya kiutendaji.
Aidha, aliitaka Menejimenti ya mamlaka hiyo kupitia upya mkataba wa mzabuni aliyeagiza vifaa hivyo kuona kama wataweza kunusuru kiasi cha fedha zilizotumika.
“Kuna haja ya kuupitia upya mkataba wa mzabuni tuone kama kuna njia yoyote ya kuokoa zile fedha lakini bado tuendelee pia kuangalia namna ya haya matishari yatakavyotumika kwa njia mbadala.
"Kama alivyosema Waziri Mkuu (juzi) nasisitiza kwamba aliyehusika tutamshughulikia.”
Mhandisi Ngonyani alisisitiza kuwa wananchi wajenge imani na serikali ya awamu ya tano kwamba Bandari mpya ya Mwambani itajengwa na kamwe haitakuwa ndoto; hatua itakayoenda sambamba na ujenzi wa njia ya reli kutoka Tanga mpaka Musoma.
Awali, Kaimu Meneja wa TPA Mkoa wa Tanga, Kapteni Andrew Matillya alisema kwa wastani wa kila mwezi Meli ya moja ya shehena ya mafuta inapukuliwa bandarini hapo na kwamba utaratibu unaotumika kupima mafuta hayo si wa flow meters kwani ziliondolewa tangu mwaka 2011.
“Kila mwezi kuna wastani wa meli moja inapakua mafuta kwenye bandari hii lakini utaratibu unaotumika ni wa bye-pass kwa maana kwamba flow meters hazitumiki kupima kiasi cha mafuta kinachoingia nchini,” alisema.
Naye Mbunge wa Jimbo la Tanga, Mussa Mbaruku (CUF), aliishukuru serikali ya awamu ya tano kwa hatua mbalimbali inazochukua kama kurudisha matumizi ya Flow meters na ahadi ya ujenzi wa bandari ya Mwambani.
Alisema maamuzi hayo yanajenga matumaini mapya kwa wananchi wa Tanga ambao walishakata tamaa.
Hivi karibuni Serikali ilimsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari, Bernadina Mwijarubi.
Mwijarubi ndiye anashughulikia kitengo cha mafuta bandarini.
MAAJABU YA MTANDAONI BOFYA HAPO CHINI HUTAAMINI MACHO YAKO.
ABOUT PRINCE BEWISA: PRINCE BEWISA BLOG is an independent organization which belongs to Bewisa Multimedia and Communication (BMC Media). Prince Bewisa was officially established on September 25, 2013 for the purpose of publishing Social contents that benefits to every visitor and community in general. It’s social blog for News, Entertainments, Education, Sports, Articles, and Business.
Post a Comment