Featured
Loading...

Waziri Mkuu Awataka Viongozi Wa Dini Kushirikiana Na Serikali Kupambana Na Rushwa, Ufisadi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili zikiwemo za rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Amesema siku zote kumekuwa na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na Asasi mbalimbali ikiwa ni pamoja na madhehebu ya Dini katika kuwapatia huduma za kijamii kama vile, afya, elimu, maji, utunzaji wa mazingira na nyingi nyingine.

Waziri Mkuu Majaliwa aliyasema hayo jana mchana (Jumapili, Juni 12, 2016) wakati alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli katika Ibada ya kuwekwa wakfu  na kusimikwa kuwa Mhashamu  Askofu Flavian Kassala kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Geita.

“Serikali inatambua jitihada kubwa zilizowekwa na Kanisa Katoliki katika Jimbo hili la Geita na Tanzania kwa ujumla hivyo wito wangu kwa Baba Askofu na Waumini wa Kanisa kwa ujumla wenu ni kuwaomba muendelee na kazi hii nzuri ya kutoa huduma muhimu kwa jamii,”alisema.

Alisema maendeleo ya nchi yanawategemea wote hivyo ushirikiano  kati ya Kanisa na Serikali utawezesha maendeleo ya Taifa kupatikana kwa kasi zaidi na kunufaisha wananchi wote.

Waziri Mkuu alisema jukumu la Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ambayo yatasaidia Mtanzania kujikomboa na umaskini na kwamba kazi kubwa ya viongozi wa dini kuunganisha jamii na wala siyo kuwatenganisha.

Hata hivyo Waziri Mkuu alisema kinachotakiwa kufanywa na wote ni kumwuomba Mwenyezi Mungu awawezesha kuwaelewa viongozi walioko madarakani na kutii maelekezo yanayotolewa kwani hata vitabu vya dini vinaelekeza kutii mamlaka.

Alisema iwapo waumini watatii na kuzingatia mafundisho ya kiroho yanayotolewa na viongozi wao wa dini ni dhahiri kwamba yatajenga imani miongoni mwao na upendo utatawala katika jamii nzima.

Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kushirikiana na Madhehebu yote katika kuwahudumia Watanzania wote bila ubaguzi, hivyo aliwasihi waendelee kuwekeza katika huduma za jamii ikiwemo Shule, Vyuo, Zahanati kwa kuwa wana jukumu la kushirikiana kwa pamoja kujenga taifa.

Wakati huo huo Waziri Mkuu aliwaomba wote kwa pamoja waunge mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli katika kupambana na uzembe, ubadhirifu na wote wanao kiuka maadili ya utendaji wa kazi.

Kwa upande wake Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo la Bunda ambaye alikuwa msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki Geita amewaomba waumini kumpa ushirikiano Askofu mpya wa jimbo hilo.
  
 IMETOLEWA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, JUNI 12, 2016.

MAAJABU YA MTANDAONI BOFYA HAPO CHINI HUTAAMINI MACHO YAKO.

ABOUT PRINCE BEWISA: PRINCE BEWISA BLOG is an independent organization which belongs to Bewisa Multimedia and Communication (BMC Media). Prince Bewisa was officially established on September 25, 2013 for the purpose of publishing Social contents that benefits to every visitor and community in general. It’s social blog for News, Entertainments, Education, Sports, Articles, and Business.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UHURU WA MAWAZO | Designed By Code Nirvana
Back To Top