Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamemgeuka Rais Dk. John Magufuli na kutaka kasi yake iangaliwe upya vinginevyo inaweza kukigharimu chama hicho tawala kwa wananchi.
Tangu Rais Magufuli aingie madarakani kumekuwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa ikiwamo kuifumua Bandari ya Dar es Salaam na kusimamisha vigogo kadhaa pamoja na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahaco) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hatua nyingine ni kubomoa nyumba katika bonde la Msimbazi na Mkwajuni jijini Dar es Salaam na kuwafukuza wafanyakazi wageni wasio na vibali.
Wakizungumza katika vikao vya siri vilivyoanza mjini Dodoma tangu juzi na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, baadhi ya wabunge wanaelezwa kuonyesha hofu ya hatua hizo kuwa huenda zitakigharimu chama chao kwa wananchi.
Wabunge hao wapo mjini Dodoma kwa ajili ya semina ya siku mbili yenye lengo la kupata mbinu za kupambana na kambi ya upinzani ambayo imefanikiwa kuongeza idadi ya wabunge katika Bunge la 11 litakaloanza rasmi wiki ijayo.
Taarifa kutoka chanzo cha uhakika ndani ya vikao hivyo, zilisema kuwa wabunge hao walilalamikia suala la bomoabomoa kwamba linakichafua chama chao mbele ya wananchi na kuhoji kama hakukuwa na njia nyingine za kuwahamisha wananchi hao.
“Wabunge wametaka ubomoaji usitishwe kwa waliojenga ndani ya mita 60, ila afadhali ufanywe kwa walio mabondeni kabisa. Wengine walishauri kuwa ubomoaji ungeachwa kabisa hadi mvua zianze ndipo wawaondoe,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo chetu kilisema kutokana na hoja za wabunge hao, ilimlazimu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kulazimika kusimama na kuanza kutetea suala la bomoabomoa na kusema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa ili kuwanusuru wananchi na mafuriko wakati wa masika.
“Hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju naye alisisitiza kuwa Serikali inafuata sheria katika ubomoaji huo, huku akiwatoa hofu kwamba uamuzi huo hautakiathiri chama,” kilisema chanzo chetu ndani ya vikao hivyo.
Mbali na bomoabomoa ambayo inaendelea, masuala mengine yaliyoibuka katika semina hiyo ni pamoja na kuwabana wawekezaji na wafanyabiashara kiasi cha kuwabughudhi.
“Wabunge wameitaka Serikali isiwajengee hofu wafanyabiashara na wawekezaji katika kulipa kodi, bali watazamwe ili wasione mazingira magumu ya kufanya biashara,” kilisema chanzo.
Kutokana na hali hiyo, wabunge walimtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kukutana na wafanyabiashara na sekta binafsi ili kuwarudishia imani.
Mwishoni mwa mwaka jana, Rais Magufuli alikutana na wawakilishi wa sekta binafsi jijini Dar es Salaam.
Suala jingine lililojadiliwa kwenye vikao hivyo ni la kuwaruhusu wabunge wa kuteuliwa kuingia kwenye uchaguzi wa mameya, hasa kwa Jiji la Dar es Salaam ambalo Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene alilitolea ufafanuzi.
Akizungumza na wabunge hao, Katibu Mkuu wa CCM, Kinana, aliwataka kutobweteka na kuitetea Serikali bali waibane na kuondoa sheria kandamizi za kikoloni.
“Kinana amewaambia wabunge wa CCM wasipokuwa wakali katika kuibana Serikali watakiponza chama na kukifanya kianguke. Kinana ametuagiza tupambane kuondoa sheria kandamizi ikiwamo kupunguza kodi ya mafuta.
“Amesema tabia ya kuwaachia wapinzani ndio waibane Serikali iachwe na badala yake kila mtu awe mwiba,” kilisema chanzo.
Pamoja na hali hiyo wabunge hao pia walijadili hatima ya vyombo vya habari nchini ambapo walitaka wamiliki wa vyombo hivyo kuwalipa mishahara mizuri waandishi wa habari na vikishindwa vijiondoe vyenyewe kwenye biashara hiyo.
Wametaka pia Serikali itunge sheria itakayoweka viwango vya elimu kwa waandishi wa habari ili kuondoa usumbufu kwa waandishi wasio na sifa.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM Bara, Pius Msekwa, aliyetoa mada ya ‘Wajibu wa mbunge wa CCM katika mfumo wa vyama vingi’ alieleza jinsi kambi ya upinzani bungeni inavyokuwa na mkakati wa kuidhoofisha Serikali ili katika uchaguzi wachukue madaraka.
Aliwataka wabunge wa CCM kutafuta mbinu madhubuti za kujilinda na kujitetea ili kuzuia hilo lisitokee.
Alisema ni wajibu wa kila mbunge wa CCM kuiwezesha Serikali ya chama chake kutekeleza majukumu yaliyoahidiwa katika ilani ya uchaguzi kwa kupitisha miswada ya sheria inayowasilishwa na Serikali kwa madhumuni hayo ikiwamo bajeti zinazopendekezwa.
“Kwahiyo ni halali kabisa kwa wabunge wa CCM kutumia uwingi wao kuidhinisha maombi ya bajeti yanayoletwa bungeni na Serikali ili kuiwezesha nayo itimize ahadi zilizotolewa kwa wananchi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya chama,” ilisema sehemu ya mada ya Msekwa.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu vikao hivyo, Katibu wa wabunge wa CCM ambaye pia ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Vijana, Jenister Mhagama, alisema hivyo vilikuwa vikao vya chama hivyo anayepaswa kuzungumzia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Naye Nape alipoulizwa kuhusu vikao hivyo, alisema hawezi kuzungumza kwa kuwa ni vya siri.
ABOUT PRINCE BEWISA: PRINCE BEWISA BLOG is an independent organization which belongs to Bewisa Multimedia and Communication (BMC Media). Prince Bewisa was officially established on September 25, 2013 for the purpose of publishing Social contents that benefits to every visitor and community in general. It’s social blog for News, Entertainments, Education, Sports, Articles, and Business.
Post a Comment